Monday, February 16, 2015

Mwanariadha wa mbio ndeffu Hyvon Ngetich alimaliza mita 50 za mwisho kwa kutambaa



Ingawa mwanariadha wa masafa marefu kutoka Kenya Hyvon Ngetich hakufanikiwa kushinda mbio za masafa marefu za Austin mwaka huu bila shaka alifanikiwa kuteka nyoyo za watu kutokana na ujasiri wake wa kutambaa na kuhakikisha kuwa amemaliza mbio hizo. 
Hyvon Ngetich mwenye umri wa miaka 29, aliishiwa na nguvu akiwa mita 50 kutoka kwenye mstari wa kumalizia mbio hizo na hakuweza tena kuinuka na kukimbia. Mwanariadha huyo aliamua kutambaa hadi mwisho wa mbiu hizo jambo lililowashangaza na hata kuwaliza wengi waliotazama jitihada zake. 
Muuguzi mmoja alimfuata kwa karibu mkimbiaji huyo akiwa tayari kumsaidia iwapo angeishiwa kabisa. Muuguzi huyo hata hivyo hakumgusa wala kumpatia msaada wowote Ngetich jambo ambalo lingesababisha jitihada zake kukataliwa.
Akiongea kuhusu jambo hili la kushangaza Mkurugenzi wa mashindano hayo ya Austin, John Conley alisema kuwa hajawahi kuona jambo kama hilo katika miaka 43 aliyohusika na mbio za masafa marefu. 
John Conley aliyezungumza na Ngetich baada ya kumaliza mbio hizo alimwambia kuwa alikuwa ameonyesha ujasiri mkubwa katika kukimbia na kutambaa kwake. Conley aliahidi kumpa Ngetich tuzo sawa na mshindi wa nafasi ya pili licha ya kumaliza wa 3 kwani alikuwa katika nafasi ya 2 alipoanza kutambaa. 
Ngetich alimaliza katika nafasi ya 3 kwa muda wa 3:04:02, nyuma ya mshindi wa mashindano hayo Cynthia Jerop kutoka Kenya vile vile aliyemaliza kwa muda wa 2:54:21 na Mmarekani Hannah Steffan aliyemaliza wa 2 kwa muda wa 3:03:69.

No comments:

Post a Comment